Kwanza, nitaanza na wanene wenzangu wanaohonga Mafyatu mchana kweupe wakichangia miradi iwe ni ya mahekalu ya kitapeli yaitwayo ya Sir God na mengine. Lugha za munene mkuu xyz anamwaga njuluku nataka ife haraka sana. Hizo njuluku kazipata wapi na vipi kama siyo kwa kupiga? Kwanini kila anayeukwaa unene anaanza kuwa na ‘huruma’ hadi kumwaga njuluku zetu kama vile ni zake? Mbona akina mzee Nchonga, pamoja na kukaa kwenye maulaji na kufanya makubwa, walikufa makapuku? Tunamdanganya nani ili iweje na kwanini?
Tuanze na sisi wanene ili kuonyesha uongozi na uwajibikaji na si uongo na usanii. Lazima tuongoze tokea mbele na si nyuma. Je, njuluku tunayotumia na kufuja tunaipata kihalali au ni jinai inayoanza kuhalalishwa? Haiwezekani mafisi, mafisadi, na majizi yatukoge na mabulungutu ya noti ilhali wengi wanakufa kwa mabulungutu ya hasira na ukapuku. Lazima watueleze na tuelewe ‘miujiza’ wanayotenda hadi kuwa wakwasi hivi.
Naona yule anatikisa kichwa na kusonya kwa ufyosi. Ukome. Tueleze tuelewe ulivyochuma hiyo njuluku mnayofanya ikose thamani kwa manavyoigawa. Nataka kuchukua hatua hizi madhubuti si kwa sababu ya husda wala wivu. Nachelea kuingizwa cha kike na wauza mihadarati, watakatishaji njuluku, majambazi, mafisi, na mafisadi wanaotuumiza na kujidai kutusaidia kwa kumwaga njuluku kwenye matukio ya kishakunaku na kilimbukeni.
Hivi kweli inawezekanaje wakati huu ambapo mchizani Tarampu amesababisha kupanda bei ya wese na kuathiri kila kitu kupata njuluku ya kumwaga kama njugu? Kweli, mmejua kututenda! Kama nyinyi ni wakwasi na wakarimu hivi, kwanini hizo njuluku msizipeleke kunakostahiki? Hamuoni mahospitali na mashule yetu yalivyo kwenye hali mbaya?
Tuache uzwazwa, roho mbaya na uroho. Utakuta jitu ambalo ni toto la kapuku lilololalia ngozi ya kondoo likijilimbikizia na kufuja mali za Mafyatu bila huruma halafu linajionyesha kwenye matukio uchwara kuwa lina njuluku na upendo! Mingine utaiona imejiwekea misafara mirefu ya ndinga na ving’ora ili kuepa misongamano liliyoisababisha kutokana na upofu, uroho, na ulimbukeni mbali na ufisadi na ukosefu wa uadilifu na ubunifu. Kwani, hatuwaoni? Mifyatu mifisi na mifisadi inaleta miradi ya kipigaji na kufanya maisha yawe magumu. Miundombinu yetu ni mibovu. Misongamano inazidi kutusonga hadi tunakuwa na msongo wa hasira na mawazo halafu inakuja mijizi na mijambazi kutokoga kwa njuluku zetu! Mkome kabla ya Mafyatu hawajakomaa, kufyatuka na kuwakomesha kwa kuwafyatua ili muache kuwafyatua kizwazwa.
Licha ya kutaka kuanzisha lifestyle audit, nataka Mafyatu wafyatuke na kuuliza kama hawa wanaomwaga njuluku wanalipa kodi vilivyo. Pia, lazima Mafyatu wafyatuke na kujua kodi walipazo zinatumikaje. Je, zinaleta matokeo tegemewa na stahiki? Je, wahusika wanaweza kutuonyesha vyanzo vya ukwasi huu mchafu na wenye utata?
Kwa vile mie ni profesa wa uchumi, nataka kuhakikisha Fyatuland haigeuzwi kaya ya ubishororo na ulimbukeni. Haiwezekani kaya kapuku inayoishi kwa kubomubomu na kukopa kopa ikawa na mabilionea wa kuibuka ghafla bin vu bila Fyatu mkuu kufyatuka na kuwafyatua. Natitachukua hatua zitakazowafyatua mafyatu kufyatuka na kufyatua wawafyatuao ili haki ifanyike na kweli ijulikane. Fyatuland haiwezi kuwa kaya ya kambale ambapo kila mmoja ana sharubu. Nitazikata hizi sharubu uchwara na zenye kutia shaka.
Juzi, wakati fisadi mmoja mnene akipaki alionunua kwa kupiga njuluku za Mafyatu ndege alimnyea wakati akishuka. Kumbe na hayawani wanachukia ufujaji wanaofanyiwa Mafyatu wasiofyatuka hadi wanajirhusu kufyatuliwa tena kifala! Mtaani kwake, kila arejeapo, kunguru humzomea sana. Kumbe hata ndege wamefyutaka hadi kuchukia machukizo na makufuru wanayoshuhudia baadhi ya Mafyatu wakifanya kwa kutapanya njuluku!
Kama haitoshi, kuna Fyatu alijifyatua na kuniita jizi na jambazi nambari moja kwa sababu alisema kuwa nina mamlaka ya kukomesha ujambazi huu wa wazi lakini sifanyi hivyo kutokana kuwa mshirika mkuu. Alihoji nashindwa wapi wakati taknolojia imerahisisha kwa kukamata ushahidi unaoweza kutumika dhidi ya wahalifu hawa wanaojifanya wanazo. Alinipa hadi clips zilizojaa mtandaoni zikiwaonyesha hawa majambazi wakimwaga njuluku. Aliongeza kuwa kuna majambazi yanashinda baa bila kujulikana yafanyapo kazi wala kazi yafanyayo lakini, kwenye sherehe, yanamwaga njuluku kama hayana akili nzuri.
Nimalizie nikionya. Wote mliojijaza mitandaoni, naja. Akina Masunga kule Ngw’amapalala na Zanzui jiandae. Loh! Kumbe naweweseka usingizini!
